NACONGO RUKWA YATEMBELEA NA KUPONGEZA MIRADI YA PLAN INTERNATIONAL NKASI

 

MJUMBE WA NACONGO RUKWA ATEMBELEA NA KUPONGEZA MIRADI YA PLAN INTERNATIONAL NKASI

Mjumbe wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO) Mkoa wa Rukwa, kwa kushirikiana Ignas Kipeta na Rukwa Association of NGOs (RANGO), wamefanya ziara maalum ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Shirika la Plan International katika Mkoa wa Rukwa, hususan Wilaya ya Nkasi. Ziara hiyo imelenga kujionea utekelezaji wa miradi hiyo na mchango wake katika kuboresha huduma za kijamii.

Katika ziara hiyo, ujumbe ulitembelea Kata ya Mtenga, ambako Plan International imetekeleza mradi wa ujenzi wa Shule Shikizi ya Mtenga. Mradi huo umehusisha ujenzi wa madarasa mawili, vyoo vya kisasa, uchimbaji wa kisima cha maji safi na salama pamoja na ujenzi wa jengo la utawala. Hatua hiyo inalenga kuboresha mazingira ya elimu kwa watoto wa awali na shule za msingi.

Ujumbe huo pia ulitembelea Kata ya Kandasi katika Shule ya Msingi Malongwe, ambako walikagua ujenzi wa madarasa matatu yaliyokamilika na yako tayari kwa matumizi, yakiwa na jumla ya madawati 60, pamoja na mradi wa kisima cha maji safi na salama. Miradi hiyo imelenga kupunguza changamoto ya uhaba wa miundombinu ya elimu na maji kwa wanafunzi na jamii inayozunguka shule hiyo.

Katika kata hiyo hiyo, ujumbe ulitembelea Shule ya Msingi Kisura, ambako Plan International imekamilisha ujenzi wa vyoo viwili vya kisasa vyenye jumla ya matundu manane (8), vilivyozingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu. Mradi huo umechochea uboreshaji wa usafi wa mazingira na afya ya wanafunzi.

Ziara hiyo iliendelea katika Kata ya Mkwamba, Kijiji cha Tambaluka, ambapo Plan International imetekeleza ujenzi wa vyoo vya kisasa pamoja na mradi wa uchimbaji wa kisima cha maji, miradi inayochangia kuboresha afya, usafi wa mazingira na ustawi wa wananchi wa kijiji hicho.

Aidha, katika Shule ya Msingi Lyele, utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa vyoo vya kisasa na uchimbaji wa kisima cha maji unaendelea, huku katika Kata ya Kate, Shule ya Msingi Chine, kukitekelezwa miradi ya ujenzi wa madarasa na vyoo, yote ikilenga kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

Wajumbe wa NACONGO na RANGO wameipongeza Plan International kwa mchango wake mkubwa katika sekta za elimu, maji na usafi wa mazingira, wakibainisha kuwa miradi hiyo inaleta mabadiliko chanya na ya kudumu katika maisha ya watoto na jamii kwa ujumla. Aidha, wametoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo kuiga mfano wa Plan International kwa kushirikiana na serikali pamoja na wananchi wa vijiji husika katika kuleta maendeleo endelevu.